Search form

EFE. 5

1-Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; 2-mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

Zikataeni Njia za Kipagani

3-Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; 4-wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. 5-Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. 6-Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. 7Basi msishirikiane nao. 8-Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, 9kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; 10-mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. 11-Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; 12-kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. 13-Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. 14-Hivyo husema,

Amka, wewe usinziaye,

Ufufuke katika wafu,

Na Kristo atakuangaza.

15-Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; 16-mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. 17-Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. 18-Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; 19-mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; 20-na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;

Nyumba ya Kikristo

21-hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.

22-Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 23-Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. 24Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

25-Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; 26-ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; 27-apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. 28Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. 30-Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. 31-Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. 32-Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. 33Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index