Search form

KUT. 25

Matoleo kwa ajili ya Hema Takatifu

1-BWANA akanena na Musa, akamwambia, 2-Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. 3Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba, 4na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani safi, na singa za mbuzi; 5na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na miti ya mshita, 6na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; 7-na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. 8-Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. 9Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya.

Sanduku la Agano

10-Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. 11Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. 12Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. 13Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. 14Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. 15-Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. 16-Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. 17-Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. 18Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. 20-Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21-Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22-Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.

Meza ya Mikate iliyowekwa Mbele ya Mungu

23-Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. 24Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote. 25Kisha ifanyie upapi wa kuizunguka pande zote, upana wake utakuwa nyanda nne, nawe uufanyie ule upapi ukingo wa urembo wa dhahabu wa kuuzunguka pande zote. 26Uifanyie vikuku vinne vya dhahabu, na kuvitia vile vikuku katika pembe zake nne, katika miguu yake minne. 27Vile vikuku na viwe karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza. 28Fanya ile miti ya mti wa mshita, na kuifunika dhahabu, kwamba ile meza ichukuliwe kwayo. 29-Nawe fanya sahani zake, na miiko yake, na makopo yake, na vikombe vyake vya kumiminia; vifanye vyote vya dhahabu safi. 30-Nawe utaiweka mikate ya wonyesho juu ya meza mbele yangu daima.

Kinara cha Taa

31-Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; 32-nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili 33vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; 34na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; 35na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. 36Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. 37-Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. 38Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. 39Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. 40-Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index