Search form

MT. 24

Kuharibiwa kwa Hekalu Kwatabiriwa

1-Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. 2-Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.

Ishara za Mwisho wa Nyakati

3Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? 4Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. 5-Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. 6-Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. 7-Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. 8Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.

Mateso Yatabiriwa

9-Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. 10-Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. 11-Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 12-Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. 13-Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 14-Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.

Chukizo la Uharibifu

15-Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), 16ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; 17-naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; 18wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. 19Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! 20-Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21-Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. 22Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. 23Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. 24-Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. 25Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. 26-Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. 27Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28-Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

Kuja kwa Mwana wa Adamu

29-Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; 30-ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. 31-Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.

Funzo kutoka kwa Mtini

32Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; 33nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. 34Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. 35-Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Haja ya kuwa Waangalifu

36-Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. 37-Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38-Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, 39-wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 40-Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; 41wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42-Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. 43-Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. 44-Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

Mtumwa Mwaminifu au asiye Mwaminifu

45Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? 46Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. 47-Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. 48-Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; 49akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; 50bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, 51-atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index