Search form

ZAB. 32

Shangwe kwa Kusamehewa

Ya Daudi. Funzo

1-Heri aliyesamehewa dhambi,

Na kusitiriwa makosa yake.

2-Heri BWANA asiyemhesabia upotovu,

Ambaye rohoni mwake hamna hila.

3Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa

Kwa kuugua kwangu mchana kutwa.

4Kwa maana mchana na usiku

Mkono wako ulinilemea.

Jasho langu likakauka hata nikawa

Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.

5-Nalikujulisha dhambi yangu,

Wala sikuuficha upotovu wangu.

Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,

Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.

6-Kwa hiyo kila mtu mtauwa

Akuombe wakati unapopatikana.

Hakika maji makuu yafurikapo,

Hayatamfikia yeye.

7-Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,

Utanizungusha nyimbo za wokovu.

8-Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;

Nitakushauri, jicho langu likikutazama.

9Msiwe kama farasi wala nyumbu,

Walio hawana akili.

Kwa matandiko ya lijamu na hatamu

Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.

10-Naye mtu mwovu ana mapigo mengi,

Bali amtumainiye BWANA fadhili zitamzunguka.

11Mfurahieni BWANA;

Shangilieni, enyi wenye haki

Pigeni vigelegele vya furaha;

Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index