Search form

ZAB. 40

Shukrani kwa Kuponywa na Sala ya kutaka Msaada

Kwa mwimbishaji. Ya Daudi. Zaburi.

1Nalimngoja BWANA kwa saburi,

Akaniinamia akakisikia kilio changu.

2Akanipandisha toka shimo la uharibifu,

Toka udongo wa utelezi;

Akaisimamisha miguu yangu mwambani,

Akaziimarisha hatua zangu.

3Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,

Ndio sifa zake Mungu wetu.

Wengi wataona na kuogopa,

Nao watamtumaini BWANA

4-Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake,

Wala hakuwaelekea wenye kiburi,

Wala hao wanaogeukia uongo.

5-Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi

Miujiza yako na mawazo yako kwetu;

Hakuna awezaye kufananishwa nawe;

Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri,

Ni mengi sana hayahesabiki.

6-Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,

Masikio yangu umeyazibua,

Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

7-Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,

(Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)

8-Kuyafanya mapenzi yako,

Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;

Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.

9-Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.

Sikuizuia midomo yangu; Ee BWANA, unajua.

10-Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;

Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.

Sikuficha fadhili zako wala kweli yako

Katika kusanyiko kubwa.

11-Nawe, BWANA, usinizuilie rehema zako,

Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.

12-Kwa maana mabaya yasiyohesabika

Yamenizunguka mimi.

Maovu yangu yamenipata,

Wala siwezi kuona.

Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu,

Na moyo wangu umeniacha.

13Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa,

Ee BWANA, unisaidie hima.

14Waaibike, wafedheheke pamoja,

Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize.

Warudishwe nyuma, watahayarishwe,

Wapendezwao na shari yangu.

15Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao,

Wanaoniambia, Ewe! Ewe!

16Washangilie, wakufurahie,

Wote wakutafutao.

Waupendao wokovu wako

Waseme daima, Atukuzwe BWANA.

17-Nami ni maskini na mhitaji,

Bwana atanitunza.

Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu,

Ee Mungu wangu, usikawie.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index