Search form

ZAB. 42

KITABU CHA PILI

Hamu ya Kusaidiwa na Mungu katika Dhiki

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi.

1Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.

Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.

2-Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai,

Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?

3Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku,

Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako.

4-Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu,

Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano,

Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu,

Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.

5-Nafsi yangu, kwa nini kuinama,

Na kufadhaika ndani yangu?

Umtumaini Mungu;

Kwa maana nitakuja kumsifu,

Aliye afya ya uso wangu,

Na Mungu wangu.

6Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka,

Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.

7-Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako,

Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.

8-Mchana BWANA ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami,

Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.

9Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau?

Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

10Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu,

Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?

11Nafsi yangu, kwa nini kuinama,

Na kufadhaika ndani yangu?

Umtumaini Mungu;

Kwa maana nitakuja kumsifu,

Aliye afya ya uso wangu,

Na Mungu wangu.

Swahili Union Version

Swahili Union Version (SUV): Copyright - 1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.

Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

More Info | Version Index